MFAFANUZI
Tuesday, May 30, 2017
SIASA IONDOLEWE KWENYE MIKATABA
Friday, February 6, 2015
Asasi za kiraia zakerwa na misamaha ya kodi
Na Elias
Mhegera Januari 23, 2015
Mtandao wa Kutetea Usawa Katika Kodi
nchini Tanzania umesikitishwa na lindi la misamaha ya kodi nchini na kuziomba
mamlaka husika kuachana na mtindo huo mara moja.
Akizungumza na blog ya Mfafanuzi, kwa
niaba ya mtandao huo unaofahamika kwa jina la Tanzania Tax Justice Coalition
kwa lugha ya Kiingereza, Mratibu wa asasi ya Policy Forum Bw. Semkae Kilonzo
anasema mara nyingi kodi imekuwa ikiwaumiza wanyonge na kuwapatia unafuu mkubwa
matajiri wakubwa.
Shirika la Policy Forum ndilo
mwenyeji wa mtandao huo ambao unaundwa na wadau mbali mbali zikiwamo asasi za
kiraia na wanahabari.
“Inasikitisha kuona kwamba bado
serikali yetu inaendekeza misamaha mikubwa ya kodi wakati taifa lina hali mbaya
kiuchumi, hospitali hazina dawa, shule hazina madawati na hata baadhi ya
familia zina njaa,” anasema Kilonzo.
Kauli yake inakuja kufuatia taarifa
zilizotolewa kwenye vyombo vya habari siku ya Jumanne juma lililopita baada ya
Kamati ya Bunge ya Fedha za Umma kuelezwa kwamba kulikuwa na ongezeko la
misamaha ya kodi kwa kiwango cha zaidi ya shilingi bilioni 340 katika Mwaka wa
Fedha uliopita wa 2013/2014.
Akilizungumzia ongezeko hilo,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Rished Bade alisema
baadhi ya misamaha hiyo ilitolewa kwa makampuni yanayochunguza uwepo wa mafuta
na gesi asilia katika vina vikubwa vya bahari.
Alisema kwamba misamaha hiyo ilikuwa
kiasi cha shilingi bilioni 1.48 katika mwaka fedha wa 2012/13 na ikapanda hadi
1.82 katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ambao uliishia tarehe 30, Juni 2014.
Ongezeko hili ndilo limeleta malalamiko kutoka katika taasisi mbali mbali
nchini.
Kupatikana kwa taarifa hiyo kulikuja
katika shughuliza kawaida za kamati za Bunge, ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo
Mhe. Zitto Kabwe aliwasomea mrejesho huo wanahabari waliokuwapo katika ofisi za
Bunge jijini Dar es Salaam.
Akiizungmzia hali hiyo ofisini kwake Mikocheni
kwa Warioba, Bw Kilonzo alisema Tanzania imekuwa ikiathiriwa na ukusanyaji wa
kodi usiozingatia maadili. “Uwazi katika ukusanyaji wa kodi ni mojawapo ya
mahitaji katika dhana nzima ya utawala bora,” alisema Bw. Kilonzo.
Anaongeza, “tunaishukuru serikali
yetu kwa mipango ya kufanya mabadiliko katika kodi ya ongezeko la thamani, na
jitihada za kupunguza misamaha ya kodi, lakini ni muhimu ihakikishe kwamba kila
mmoja anachingia kwa usawa kulingana na kipato chake katika hazina ya
taifa.”
Alichukua fursa hiyo kulikumbusha
Bunge la Tanzania kukamilisha Miswaada miwili yaani Mswaada wa Ongezeko la
Thamani wa 2014, na Mswaada wa Utawala wa Kodi wa Mwaka 2014, anashauri miswada
hiyo ijadiliwe haraka ili kuondoa maduku duku.
Akiuzungumzia wa kwanza anasema
unalenga katika kubakiza misamaha katika maeneo muhimu tu baada ya kutolewa kwa
cheti cha misamaha hiyo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), baada ya
tathmini ya kina.
Bw. Kilonzo anasema ni kweli kwamba
kutokana na makubaliano ya kidiplomasia katika mikataba ambayo pia Tanzania
imeiridhia baadhi ya bidhaa za kidiplomasia hazitozwi kodi. Lakini bidhaa hizo
ni zile zilizomo katika shughuli za kiserikali tu.
Anashauri kwamba mamlaka ya waziri wa
fedha yapunguzwe au yadhibitiwe pale yanapohusika katika utoaji wa misamaha ya
kodi kwa sababu kwa njia hiyo upo uwezekano mkubwa wa misamaha hiyo kutumiwa
vibaya na hata wakati mwingine kuambatana na matumizi ya rushwa.
Kuhusu namna nyingine ya kupunguza misamaha
ya kodi anashauri kwamba kuwepo na mjadala mpana wa kina unaowahusisha wadau
mbali mbali badala ya serikali kuu kujimilikisha maamuzi yote yanayohusiana na
kodi.
Zaidi ya hayo anasema wale wote
wanaosamehewa kodi waripotiwe kwenye vyombo vya habari na sababu za misamaha
hiyo ziwekwe bayana. “Sioni sababu ya usiri katika misamaha hiyo zaidi ya
kunufaishana kwa wenye mamlaka,” anaonya.
Kuhusiana na Mswaada wa Utawala wa
Kodi wa 2014, Kilonzo anasema iwapo Mswaada huo utapitishwa na kuwa
sheria, basi sheria hiyo italeta
mapinduzi ya aina yake tokea kuanzishwa kwa mamlaka hiyo (TRA), mwaka 1995.
Anazungumzia uelewa wake katika
masuala ya kodi kutokana na mafunzo aliyoyapata kutoka katika taasisi mbali
mbali kama vile Tax Justice Network of Africa, Financial Transparency Coalition,
Global Financial Integrity n.k. na kusema siku zote misamaha mingi ya kodi
haina manufaa kwa walio wengi bali kwa makundi machache.
Akifafanua zaidi anasema wakati
mwingine kodi imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kisiasa kwa manufaa ya vyama
tawala na wakati mwingine hata kwa lengo la kuwaumiza wafanya biashara wanaounga
mkono vyama vya upinzani, na wafanya biashara wanaoonekana kwamba hawazuingi
mkono serikali zao.
“Ni jukumu letu sisi asasi za kiraia
kuelimisha umma kwamba si haki kwa serikali kutoa misamaha ya kodi kwa makubaliano
ya nipe nikupe, yaani kuwasamehe kodi wafanyabiashara wanaovichangia vyama
tawala, kodi ni mali ya wananchi wote si mali ya watawala,” anaonya.
Anasema kwamba hata katika Miswaada
iliyopelekwa bungeni bado kuna vipengele vinavyompatia mamlaka ya mwisho
Kamishna Mkuu wa TRA katika kutoa misamaha jambo ambalo bado linaweza kutumika
vibaya.
Kilonzo anasema katika mazingira ya
sasa Kamishna Mkuu wa TRA amekabidhiwa mamlaka makubwa sana ambayo yanaweza
kutumika vibaya na wenye mamlaka hususani kwa matakwa ya kisiasa.
Anashauri kwamba hata hicho
kinachoitwa kwamba ni misamaha kwa lengo la kuvutia uwekezaji nia lazima
izingatie uwazi, uwajibikaji, na haki.
“Katika ujumla wake suala la utawala
wa kodi linahitaji uwazi, maadili, na uwajibikaji siyo wa maafisa wachache
wanaopokea amri kutoka serikalini bali wanaotimiza majukumu yao kutokana na mamlaka
ya kitaasisi,” anahitimisha.
Pichani: Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bwana Rished Bade
Wednesday, January 7, 2015
MJADALA WA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW-MHARIRI EVARIST MWITUMBA USIPOTOSHWE!
Na Elias Mhegera
Kwanza naomba
nikusalimie kwa jina la Bwana muumba wa mbingu na dunia, na kisha nikutakie
heri ya mwaka mpya! Siku ya juzi niliona comments zako zikiunga mkono uchambuzi
kuhusiana na sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, sikuridhishwa na comments zako
na ndiyo maana nimeandika hoja hizi.
Nikirejea katika mada
yenyewe kuhusiana na sakata la akaunti hiyo, kwanza naomba nikiri kwamba kwa
tabia yangu binafsi huwa sipendi sana malumbano, hususani na wanataaluma
wenzangu katika jambo lolote lile.
Pili naomba nikiri
kwamba na mimi nimekuwa nikisikia fununu kwamba miongoni mwa sababu za kukuzwa
sana kwa sakata hili ni jaribio la ‘vigogo’ kadhaa kuandaa mazingira ili Prof.
Sospeter Muhongo alinyakue jimbo la Wakili, na Mbunge wa Musoma Vijijini Mhe.
Nimrod Mkono.
Inadaiwa kwamba Prof.
Muhongo analindwa kwa nguvu zote kwa sababu ni mbabe na anaweza kuendelea
kuwalinda vigogo waliohusika na ufisadi katika mikataba ya mafuta na gesi
asilia, rejea sakata la Muhongo kuwalinda watendaji wa TPDC.
Tutakwenda mbela na
kurudi nyuma, lakini jambo moja ni dhahiri, kuna ufisadi mkubwa unaowahusu
viongozi wetu wakubwa, ambao sasa tunawataka wajimalize wao wenyewe! Soma dhana
hiyo katika novel ya James Hadly Chase: You Find Him-I’ll Fix Him, hebu ichote
hapa:file:///C:/Users/USER/Desktop/james-hadley-chase-you-find-him.pdf
Novel hii inaelezea
jinsi ambavyo muovu anaaminika, na anatakiwa kuchukua hatua juu ya wale
wanaoonekana kwamba ni ‘waovu’! ni dhahiri kwamba muovu huyo atajitahidi
kuwalinda kwa nguvu zote kwani ndani ya nafsi yake anafahamu fika kwamba yeye
ndiye kawaponza hao wanaoonekana kwamba ni waovu/wahalifu-hiyo ndiyo Escrow!
kutokana na maslahi
mapana ya taifa, na pia mazingira yanayolizunguka sakata hilo mpaka sasa, nalazimika
kutoa mchango wangu, tena kwa majonzi makubwa kwa sababu nalazimika kutaja
mambo ambayo yatawagusa watu ambao kwangu siyo kwamba ni marafiki wa karibu
bali wengine ni ndugu zangu wa damu.
Hata hivyo udugu wetu
huo nisingependa unifunge mdomo wangu pale ninapoona kwamba madhara ya mimi
kukaa kimya ni makubwa kulikoni kuyaweka wazi niyafahamuyo kwa manufaa na
mustakabali wa taifa zima. Nimeisoma makala ya Kazi Msemakweli akiwatetea vilivyo
maprofesa wawili, Sospter Muhongo na Anna Tibaijuka.
Agizo la Prof Tibaijuka akitaka jengo la CCM liobomolewe ili kumpisha 'mwekezaji'
Kwa vile kauli
zifuatazo “Nashawishika kuamini ukweli
huu” na “Nimependa uchambuzi huu wa
sakata la Escrow, soma hapa” zikihusiana na makala “Sayansi ya hoja na mantiki katika Escrow Account” ni zako (Mwitumba),
mimi nakwazika kidogo, na kama nitakuwa nimekukwaza wewe pia kwa mchango wangu
basi naomba uniwie radhi.
Nakwazika kwa sababu wewe ni mwandishi mahiri na mhariri
mkongwe uliyepata kuongoza gazeti la habari za uchunguzi la This Day, ina maana
michezo iliyotumika katika kutengeneza makala ile kwa ngazi yako wewe, uzoefu
na uelewa ni sawa na mtoto wa chekechea kumfundisha profesa taaluma yake!
Maneno “NASHAWISHIKA KUAMINI UKWELI HUU???!” badala ya
“NASHAWISHIKA KUAMINI MAONI/UCHAMBUZI HUU” kidogo yanakwaza hasa yanapotoka
katika fikra pevu za mwana taaluma mkongwe kama wewe. Hivi mpaka sasa bado
unaamini kwamba kuna ukweli wowote katika sakata la Tegeta Escrow?
Unazungumzia ukweli upi? Ule unaoetetewa na Rais Kikwete, na
timu yake ya akina Prof Muhongo? Eliakim Maswi, Prof Tibaijuka n.k. je ulisoma
alichokieleza Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania? Je umeyasoma
majina ya wahusika wengine waliochota pesa hizo kama walivyoandikwa katika
toleo moja la gazeti la Jamhuri?
Kisha nairejea kauli yako nyingine: “Nimependa uchambuzi huu
wa sakata la Escrow, soma hapa” hivi hapo kuna uchambuzi kweli ndugu yangu
Mwitumba? Mimi binafsi nimeona pumba tupu zilizoandikwa na waandishi ‘mamluki’
yaani wa kukodiwa ‘hack writers’ au ‘mercenary journalists’ watu ambao hulipwa
pesa na kuandika upumbavu wowote wanaoelekezwa na mlipaji wao.
Nilitegemea kwamba kwa kuwa wewe umekaa kwenye chumba cha
habari kwa muda mrefu kuliko mimi ambaye kwa muda mwingi nimekuwa nikiandika
kama mwandishi wa kujitegemea na nimekaa katika chumba cha habari kwa muda
usiozidi miaka sita (6) mpaka sasa, ungekuwa na upeo mkubwa zaidi wa kuunganisha
mambo kulikoni mimi.
Kisha nataka nirejee
katika jina la mwandishi mwenyewe anayeitwa KAZI MSEMAKWELI, binafsi katika
taaluma yangu ya utambuzi wa majina niliyoipata wakati nikiwa Afisa Uhamiaji,
hata jina lenyewe tu lina utata na linaacha maswali mengi kuliko majibu!.
Mwandishi huyo ukiangalia jinsi alivyojenga hoja kwa hali yoyote ile ni
mwandishi mkongwe.
Lakini ukienda kwenye
facebook mtafute kwa jina hilo hapatikani, nenda tumia google search
hapatikani, basi tafuta hata picha yake tu, haipatikani!. Ni dhahiri huyo ni
mwandishi ‘ruhani’ ni mwandishi wa kutunga ‘fictitious’ au ni mwandishi jinni
kitaaluma anakaribiana mno na hao ‘ghost writers’ ambao kazi yao ni kuandika
fikra za watu wengine na wala siyo fikra zao wenyewe.
Ofisi ya jengo la CCM-Gama Makaani kabla halijabomolewa
Ukiachana na jina lake
nenda hata katika gazeti au magazeti ilipotumika makala hiyo, nimeisoma makala
hiyo nzima yenye kurasa tatu na imeelezwa kwamba ilitumika kwa mara ya kwanza
katika gazeti la Alhuda na ndipo ikahamishiwa katika gazeti la Taifa Imara.
Kimsingi magazeti haya
yote mawili yamo katika mfumo wa umiliki unaoitwa ‘Quasi-independent’ kwa maana
ya kwamba si magazeti huru bali ni magazeti huru nusu nusu! Kabla ya makala
hii, gazeti la Taifa Imara liliwahi pia kuandika kwa “Wakatoliki wakerwa kwa
maaskofu wao kudhaliishwa” uandishi wa ain hii mimi naona kwamba ni upuuzi mtu!
Ukitaka kuyafahamu kwa
vile wewe ni mtaalamu basi fanya utafiti mdogo wa ‘content analysis’ rejea
magazeti ya aina hii yaliandika nini kwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010! Kwa
mfano An-Nuur, Tazama Tanzania, Sauti ya Umma, na hata Changamoto yalijikita
katika kuandika kwamba Dkt Slaa katumwa na Kanisa katoliki, kapora mke wa mtu,
na hata kuunga mkono pale Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lilipotoa vitisho.
Tayari jengo limeishapigwa nyundo kwa amri ya Tibaijuka na zoezi hilo kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Ahmed Kipozi
Magazeti mengine
yaliyounga mkono habari hizo vikiwamo vitisho vya JWTZ ni Daily News, Uhuru,
Jambo Leo, Habari Leo, An-Nur etc. uwiano wa sera kati ya magazeti haya na yale
ya serikali na chama cha Mapinduzi ni kiashiria tosha kwamba hayo siyo magazeti
huru bali yanafadhiriwa na watawala wetu wa sasa.
Natoa mifano michache:
Tazama Tanzania Na.417, Oktoba 30, 2010 “Sababu
za kutomchagua Dk Slaa kesho hizi hapa” Tazama Tanzania Na. 419, Nov 9-15,
2010 “kwa nini Kanisa Katoliki linataka
kutupokonya Nyerere wetu?” An-Nuur 912, Septemba 28, 2010 “Tuhuma za uporaji wake za watu zitazamwe,”
na katika toleo hilo hilo: “Kikwete kawakosea nini maaskofu”
Ann Nur, Toleo Na. 903,
Septemba 17-20, 2010 “CHADEMA ya
walokole, akina Zitto mamluki?” Pia katika toleo hilo hilo “Slaa ni chaguo la Katoliki” An-Nuur Na.
903, Agosti 20-26, 2010 “Padri anaweza
kuwa mtawala bora”
Mifano ipo mingi naomba
nisiende zaidi katika hilo. Kuhusu gazeti la Taifa Imara ambalo mimi naamini
bado ni jipya, ni miongoni mwa magazeti hayo hayo niliyoyazungumzia ambayo ni
nusu huru, na yanalipwa na watawala wetu na kwa hiyo habari zake haziwezi
kuaminiwa na watu makini aina ya Bw. Evarist Mwitumba.
Kuhusu migao ya pesa za
Tegeta Escrow, kila mfuatiliaji makini atagundua kwamba huu ni muendelezo wa
sakata la EPA, kwa sababu baadhi ya wanufaika wa pesa za EPA sasa tena ni
wanufaika wa hizo za Escrow! Nani asiyefahamu kwamba Jaji Mujulizi alitokea
katika kampuni ya mawakili ya IMMMA Advocates ambao walinufaika na pesa za EPA,
mazingira ya uteuzi yake ni yapi, ni kwanini tena jaji huyu yumo kwenye mgao wa
Escrow?
Kama pesa hizo ni
halali mbona aina ya mgao uliofanyika unafuata mkondo yote ya fedha chafu
zilizotakatishwa? Mbona Askofu Kilaini ni kiongozi pekee wa Kanisa Katoliki
aliyepata kusema kuwa ‘Bw. Mafuta Mengi’
kwa kuazima msemo wa Wakenya ni chaguo la Mungu na sasa anapata mgao wa
Escrow?
Ni nani asiyefahamu
ubia wa Prof. Tibaijuka a.k.a jembe na ‘Bw Mafuta Mengi’ katika uporaji mkubwa
wa ardhi? Mfano halisi ni jinsi alivyolazimisha kugawa ardhi kwa kampuni ya
“mwekezaji bandia” ya Eco-Energy katika maeneo ya Bagamoyo?
Kwa mfano mimi
nilipofuatilia katika Idara ya Uhamiaji makao makuu afisa wa vibali vya makazi
akaniletea mafaili matano ambapo mwekezaji huyo amechukua ardhi kubwa, ambayo
hata hivyo haifanyiwi kazi yoyote zaidi ya kuwapora wakulima wanyonge.
Nilipomhoji je ni kwa
nini mwekezaji huyo anaishi Tanzania kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka huo (2014)
bila kazi yoyote ki-Uhamiaji tunamuita ni mkazi mzigo (destitute) na serikali
haijachukua hatua yoyote?
Wanakijiji wa Gama Makaani wakilalimikia kitendo cha kuporwa ardhi yao na kukabidhiwa mwekezaji wa ECO-ENERGY
Afisa huyo wa uhamiaji
akanijibu “Bw. Elias, ndugu yangu, naomba achana na jambo hili, Tanzania ya leo
siyo ya jana, unaweza kustukia mtu anakuchoma kisu chenye sumu kali mgongoni
mwako na ukapoteza maisha yako, na muuaji asipatikane!, tulia tulee watoto
ndugu yangu!” mwisho wa kumnukuu.
Kwa tafsiri yangu
mwekezaji wa Eco-Energy ni muajiriwa wa Mtanzania tajiri na mwenye mamlaka (kama
ilivyokuwa kwa IPTL, rejea kauli ya Mhe. Tundu Lissu kabla hajingiliwa na ‘Dr’
Mary Nagu, na ndiyo maana anaweza kuishi
nchini bila usumbufu na adha zozote toka Idara ya Uhamiaji.
Binafsi nimefanya
mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa Eco-Energy Bw. Anders Bergfors ofisini kwake na
pia Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Ahmed Kipozi na wote walijikanyaga tu
katika majibu yao. Kwa hiyo Prof Tibaijuka alikuwa analipwa ujira wake kwa
kufanikisha uporaji mkubwa wa ardhi haijalishi pesa hizo zilipitia miononi mwa
nani iwe Rugemalira au Ruge-maliza!
Askofu Kilaini vivyo
hivyo alikuwa anapata mgao wa shukrani kwa kusimama hadharani na kumfanyia
mwanasiasa kampeni kinyume na msimamo wa kanisa lake. Viongozi wengine kama
Askofu Nzigilwa na mapadri wanaweza kuwa wametumika tu ili kuficha lengo
hatuwezi jua labda wanaandaliwa kwa ajili ya kusaidia kampeni za 2015.
Prof. Muhongo
anafahamika kwa ubabe wake wa kukataa kutoa mikataba katika sekta ya mafuta na
gesi asilia kama sheria na mikataba ya kimataifa inavyotakiwa yaani kuwa ya
wazi badala kuwa mali na siri ya serikali pekee.
Rejea vipengele hivyo
katika African Peer Review Mechanism (APRM) na Open Government Partneship (OGP)
inavyoagiza. Kuhusu utakatishaji wa fedha ni somo ninalolifahamu kwa kina.
Nilipata mafunzo juu ya
utakatishaji wa pesa kutoka taasisi ya kupambana na utoroshaji wa watoto, yaani
African Network for The Prevention & Protection against Child Abuse and
Neglect (ANPPCAN) na mpango wa kupambana na ufadhili kwa ugaidi na uhalifu mwingine
mkubwa.
Pia nimewahi kupata
mafunzo mengine kama hayo kutoka kwa taasisi ya Financial Transparency
Coalition, chini ya asasi ya Policy Forum.
kadi ya utambulisho katika mafunzo ya uhalifu kuhusiana na fedha, kukwepa kodi na kutakatisha fedha yaliyodhaminiwa na asasi ya Policy Forum
Hivyo basi
kilichofanyika katika benki za Mkombozi na Stanbic ndiyo hicho hicho hufanyika
katika utakatishaji wa pesa chafu za kiharamia je ni kwa nini iwe hivyo? Yaani
akaunti inafunguliwa, pesa zinawekwa na kuchotwa kisha akaunti inafungwa! Bado
kuna utetezi hapo jamani? Je kweli hiyo ni pesa safi? Kwa nini iondolewe katika
njia chafu? Njia za hofu hofu?
Unaweza kusoma kitabu
cha Paul Allan Schott: Reference Guide to Anti-Money Laundering and Combating
the Financing of Terrorism, kwa uelewa zaidi kipate hapa: http://siteresources.worldbank.org/EXTAML/Resources/3965111146581427871/Reference_Guide_AMLCFT_2ndSupplement.pdf
Hitimisho
Naamini wasomaji
watapata mwanga ni kwa nini maprofesa hao ‘majembe’ wamekuwa na viburi na
kujiamini sana ni kwa sababu wanajiona kwamba wao wazijua siri za ‘wakubwa’ kwa
undani zaidi, yaani Muhongo katika suala la mikataba ya mafuta na gesi asilia
na Tibaijuka kuhusu uporaji mkubwa wa ardhi sehemu mbali mbali za nchii (rejea
lugha ya tulimuita, tukazungumza tukamuomba…)
MUNGU IBARIKI AFRIKA,
MUNGU UBARIKI TANZANIA
Mwandishi wa uchambuzi huu ni mkurugenzi wa utafiti na uchunguzi kutoka chama cha waandishi wa habari za haki za binadamu-JOURNORIGHTS
Wednesday, December 17, 2014
Subscribe to:
Posts (Atom)





.bmp)