Friday, February 6, 2015

Asasi za kiraia zakerwa na misamaha ya kodi
Na Elias Mhegera                   Januari 23, 2015
Mtandao wa Kutetea Usawa Katika Kodi nchini Tanzania umesikitishwa na lindi la misamaha ya kodi nchini na kuziomba mamlaka husika kuachana na mtindo huo mara moja.
Akizungumza na blog ya Mfafanuzi, kwa niaba ya mtandao huo unaofahamika kwa jina la Tanzania Tax Justice Coalition kwa lugha ya Kiingereza, Mratibu wa asasi ya Policy Forum Bw. Semkae Kilonzo anasema mara nyingi kodi imekuwa ikiwaumiza wanyonge na kuwapatia unafuu mkubwa matajiri wakubwa.
Shirika la Policy Forum ndilo mwenyeji wa mtandao huo ambao unaundwa na wadau mbali mbali zikiwamo asasi za kiraia na wanahabari.
“Inasikitisha kuona kwamba bado serikali yetu inaendekeza misamaha mikubwa ya kodi wakati taifa lina hali mbaya kiuchumi, hospitali hazina dawa, shule hazina madawati na hata baadhi ya familia zina njaa,” anasema Kilonzo.
Kauli yake inakuja kufuatia taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari siku ya Jumanne juma lililopita baada ya Kamati ya Bunge ya Fedha za Umma kuelezwa kwamba kulikuwa na ongezeko la misamaha ya kodi kwa kiwango cha zaidi ya shilingi bilioni 340 katika Mwaka wa Fedha uliopita wa 2013/2014.
Akilizungumzia ongezeko hilo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Rished Bade alisema baadhi ya misamaha hiyo ilitolewa kwa makampuni yanayochunguza uwepo wa mafuta na gesi asilia katika vina vikubwa vya bahari.
Alisema kwamba misamaha hiyo ilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.48 katika mwaka fedha wa 2012/13 na ikapanda hadi 1.82 katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ambao uliishia tarehe 30, Juni 2014. Ongezeko hili ndilo limeleta malalamiko kutoka katika taasisi mbali mbali nchini.
Kupatikana kwa taarifa hiyo kulikuja katika shughuliza kawaida za kamati za Bunge, ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Zitto Kabwe aliwasomea mrejesho huo wanahabari waliokuwapo katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.
Akiizungmzia hali hiyo ofisini kwake Mikocheni kwa Warioba, Bw Kilonzo alisema Tanzania imekuwa ikiathiriwa na ukusanyaji wa kodi usiozingatia maadili. “Uwazi katika ukusanyaji wa kodi ni mojawapo ya mahitaji katika dhana nzima ya utawala bora,” alisema Bw. Kilonzo.

Anaongeza, “tunaishukuru serikali yetu kwa mipango ya kufanya mabadiliko katika kodi ya ongezeko la thamani, na jitihada za kupunguza misamaha ya kodi, lakini ni muhimu ihakikishe kwamba kila mmoja anachingia kwa usawa kulingana na kipato chake katika hazina ya taifa.” 
Alichukua fursa hiyo kulikumbusha Bunge la Tanzania kukamilisha Miswaada miwili yaani Mswaada wa Ongezeko la Thamani wa 2014, na Mswaada wa Utawala wa Kodi wa Mwaka 2014, anashauri miswada hiyo ijadiliwe haraka ili kuondoa maduku duku.
Akiuzungumzia wa kwanza anasema unalenga katika kubakiza misamaha katika maeneo muhimu tu baada ya kutolewa kwa cheti cha misamaha hiyo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), baada ya tathmini ya kina.
Bw. Kilonzo anasema ni kweli kwamba kutokana na makubaliano ya kidiplomasia katika mikataba ambayo pia Tanzania imeiridhia baadhi ya bidhaa za kidiplomasia hazitozwi kodi. Lakini bidhaa hizo ni zile zilizomo katika shughuli za kiserikali tu.
Anashauri kwamba mamlaka ya waziri wa fedha yapunguzwe au yadhibitiwe pale yanapohusika katika utoaji wa misamaha ya kodi kwa sababu kwa njia hiyo upo uwezekano mkubwa wa misamaha hiyo kutumiwa vibaya na hata wakati mwingine kuambatana na matumizi ya rushwa.
Kuhusu namna nyingine ya kupunguza misamaha ya kodi anashauri kwamba kuwepo na mjadala mpana wa kina unaowahusisha wadau mbali mbali badala ya serikali kuu kujimilikisha maamuzi yote yanayohusiana na kodi.
Zaidi ya hayo anasema wale wote wanaosamehewa kodi waripotiwe kwenye vyombo vya habari na sababu za misamaha hiyo ziwekwe bayana. “Sioni sababu ya usiri katika misamaha hiyo zaidi ya kunufaishana kwa wenye mamlaka,” anaonya.
Kuhusiana na Mswaada wa Utawala wa Kodi wa 2014, Kilonzo anasema iwapo Mswaada huo utapitishwa na kuwa sheria,  basi sheria hiyo italeta mapinduzi ya aina yake tokea kuanzishwa kwa mamlaka hiyo (TRA), mwaka 1995.
Anazungumzia uelewa wake katika masuala ya kodi kutokana na mafunzo aliyoyapata kutoka katika taasisi mbali mbali kama vile Tax Justice Network of Africa, Financial Transparency Coalition, Global Financial Integrity n.k. na kusema siku zote misamaha mingi ya kodi haina manufaa kwa walio wengi bali kwa makundi machache.
Akifafanua zaidi anasema wakati mwingine kodi imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kisiasa kwa manufaa ya vyama tawala na wakati mwingine hata kwa lengo la kuwaumiza wafanya biashara wanaounga mkono vyama vya upinzani, na wafanya biashara wanaoonekana kwamba hawazuingi mkono serikali zao.
“Ni jukumu letu sisi asasi za kiraia kuelimisha umma kwamba si haki kwa serikali kutoa misamaha ya kodi kwa makubaliano ya nipe nikupe, yaani kuwasamehe kodi wafanyabiashara wanaovichangia vyama tawala, kodi ni mali ya wananchi wote si mali ya watawala,” anaonya.
Anasema kwamba hata katika Miswaada iliyopelekwa bungeni bado kuna vipengele vinavyompatia mamlaka ya mwisho Kamishna Mkuu wa TRA katika kutoa misamaha jambo ambalo bado linaweza kutumika vibaya.
Kilonzo anasema katika mazingira ya sasa Kamishna Mkuu wa TRA amekabidhiwa mamlaka makubwa sana ambayo yanaweza kutumika vibaya na wenye mamlaka hususani kwa matakwa ya kisiasa.
Anashauri kwamba hata hicho kinachoitwa kwamba ni misamaha kwa lengo la kuvutia uwekezaji nia lazima izingatie uwazi, uwajibikaji, na haki.
“Katika ujumla wake suala la utawala wa kodi linahitaji uwazi, maadili, na uwajibikaji siyo wa maafisa wachache wanaopokea amri kutoka serikalini bali wanaotimiza majukumu yao kutokana na mamlaka ya kitaasisi,” anahitimisha.

 Pichani: Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bwana Rished Bade