Asasi za kiraia zakerwa na misamaha ya kodi
Na Elias
Mhegera Januari 23, 2015
Mtandao wa Kutetea Usawa Katika Kodi
nchini Tanzania umesikitishwa na lindi la misamaha ya kodi nchini na kuziomba
mamlaka husika kuachana na mtindo huo mara moja.
Akizungumza na blog ya Mfafanuzi, kwa
niaba ya mtandao huo unaofahamika kwa jina la Tanzania Tax Justice Coalition
kwa lugha ya Kiingereza, Mratibu wa asasi ya Policy Forum Bw. Semkae Kilonzo
anasema mara nyingi kodi imekuwa ikiwaumiza wanyonge na kuwapatia unafuu mkubwa
matajiri wakubwa.
Shirika la Policy Forum ndilo
mwenyeji wa mtandao huo ambao unaundwa na wadau mbali mbali zikiwamo asasi za
kiraia na wanahabari.
“Inasikitisha kuona kwamba bado
serikali yetu inaendekeza misamaha mikubwa ya kodi wakati taifa lina hali mbaya
kiuchumi, hospitali hazina dawa, shule hazina madawati na hata baadhi ya
familia zina njaa,” anasema Kilonzo.
Kauli yake inakuja kufuatia taarifa
zilizotolewa kwenye vyombo vya habari siku ya Jumanne juma lililopita baada ya
Kamati ya Bunge ya Fedha za Umma kuelezwa kwamba kulikuwa na ongezeko la
misamaha ya kodi kwa kiwango cha zaidi ya shilingi bilioni 340 katika Mwaka wa
Fedha uliopita wa 2013/2014.
Akilizungumzia ongezeko hilo,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Rished Bade alisema
baadhi ya misamaha hiyo ilitolewa kwa makampuni yanayochunguza uwepo wa mafuta
na gesi asilia katika vina vikubwa vya bahari.
Alisema kwamba misamaha hiyo ilikuwa
kiasi cha shilingi bilioni 1.48 katika mwaka fedha wa 2012/13 na ikapanda hadi
1.82 katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ambao uliishia tarehe 30, Juni 2014.
Ongezeko hili ndilo limeleta malalamiko kutoka katika taasisi mbali mbali
nchini.
Kupatikana kwa taarifa hiyo kulikuja
katika shughuliza kawaida za kamati za Bunge, ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo
Mhe. Zitto Kabwe aliwasomea mrejesho huo wanahabari waliokuwapo katika ofisi za
Bunge jijini Dar es Salaam.
Akiizungmzia hali hiyo ofisini kwake Mikocheni
kwa Warioba, Bw Kilonzo alisema Tanzania imekuwa ikiathiriwa na ukusanyaji wa
kodi usiozingatia maadili. “Uwazi katika ukusanyaji wa kodi ni mojawapo ya
mahitaji katika dhana nzima ya utawala bora,” alisema Bw. Kilonzo.
Anaongeza, “tunaishukuru serikali
yetu kwa mipango ya kufanya mabadiliko katika kodi ya ongezeko la thamani, na
jitihada za kupunguza misamaha ya kodi, lakini ni muhimu ihakikishe kwamba kila
mmoja anachingia kwa usawa kulingana na kipato chake katika hazina ya
taifa.”
Alichukua fursa hiyo kulikumbusha
Bunge la Tanzania kukamilisha Miswaada miwili yaani Mswaada wa Ongezeko la
Thamani wa 2014, na Mswaada wa Utawala wa Kodi wa Mwaka 2014, anashauri miswada
hiyo ijadiliwe haraka ili kuondoa maduku duku.
Akiuzungumzia wa kwanza anasema
unalenga katika kubakiza misamaha katika maeneo muhimu tu baada ya kutolewa kwa
cheti cha misamaha hiyo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), baada ya
tathmini ya kina.
Bw. Kilonzo anasema ni kweli kwamba
kutokana na makubaliano ya kidiplomasia katika mikataba ambayo pia Tanzania
imeiridhia baadhi ya bidhaa za kidiplomasia hazitozwi kodi. Lakini bidhaa hizo
ni zile zilizomo katika shughuli za kiserikali tu.
Anashauri kwamba mamlaka ya waziri wa
fedha yapunguzwe au yadhibitiwe pale yanapohusika katika utoaji wa misamaha ya
kodi kwa sababu kwa njia hiyo upo uwezekano mkubwa wa misamaha hiyo kutumiwa
vibaya na hata wakati mwingine kuambatana na matumizi ya rushwa.
Kuhusu namna nyingine ya kupunguza misamaha
ya kodi anashauri kwamba kuwepo na mjadala mpana wa kina unaowahusisha wadau
mbali mbali badala ya serikali kuu kujimilikisha maamuzi yote yanayohusiana na
kodi.
Zaidi ya hayo anasema wale wote
wanaosamehewa kodi waripotiwe kwenye vyombo vya habari na sababu za misamaha
hiyo ziwekwe bayana. “Sioni sababu ya usiri katika misamaha hiyo zaidi ya
kunufaishana kwa wenye mamlaka,” anaonya.
Kuhusiana na Mswaada wa Utawala wa
Kodi wa 2014, Kilonzo anasema iwapo Mswaada huo utapitishwa na kuwa
sheria, basi sheria hiyo italeta
mapinduzi ya aina yake tokea kuanzishwa kwa mamlaka hiyo (TRA), mwaka 1995.
Anazungumzia uelewa wake katika
masuala ya kodi kutokana na mafunzo aliyoyapata kutoka katika taasisi mbali
mbali kama vile Tax Justice Network of Africa, Financial Transparency Coalition,
Global Financial Integrity n.k. na kusema siku zote misamaha mingi ya kodi
haina manufaa kwa walio wengi bali kwa makundi machache.
Akifafanua zaidi anasema wakati
mwingine kodi imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kisiasa kwa manufaa ya vyama
tawala na wakati mwingine hata kwa lengo la kuwaumiza wafanya biashara wanaounga
mkono vyama vya upinzani, na wafanya biashara wanaoonekana kwamba hawazuingi
mkono serikali zao.
“Ni jukumu letu sisi asasi za kiraia
kuelimisha umma kwamba si haki kwa serikali kutoa misamaha ya kodi kwa makubaliano
ya nipe nikupe, yaani kuwasamehe kodi wafanyabiashara wanaovichangia vyama
tawala, kodi ni mali ya wananchi wote si mali ya watawala,” anaonya.
Anasema kwamba hata katika Miswaada
iliyopelekwa bungeni bado kuna vipengele vinavyompatia mamlaka ya mwisho
Kamishna Mkuu wa TRA katika kutoa misamaha jambo ambalo bado linaweza kutumika
vibaya.
Kilonzo anasema katika mazingira ya
sasa Kamishna Mkuu wa TRA amekabidhiwa mamlaka makubwa sana ambayo yanaweza
kutumika vibaya na wenye mamlaka hususani kwa matakwa ya kisiasa.
Anashauri kwamba hata hicho
kinachoitwa kwamba ni misamaha kwa lengo la kuvutia uwekezaji nia lazima
izingatie uwazi, uwajibikaji, na haki.
“Katika ujumla wake suala la utawala
wa kodi linahitaji uwazi, maadili, na uwajibikaji siyo wa maafisa wachache
wanaopokea amri kutoka serikalini bali wanaotimiza majukumu yao kutokana na mamlaka
ya kitaasisi,” anahitimisha.
Pichani: Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bwana Rished Bade

No comments:
Post a Comment